Tuesday, June 2, 2015

Rafiki ni mtu gani?, Kwanini tuna marafiki?, Je rafiki uliyenaye ni wa kweli?, Je mnaendana? Utajuaje kama rafiki yako ni sahihi au lah. Endelea kusoma hapa ......


Ni wazi kwamba kila mmoja wetu ana marafiki/rafiki aliwapata katika nyakati mbalimbali za maisha yake ya kila siku. Na pengine hata sisi wenyewe tunashindwa kuonekana kama marafiki wa kweli kwa wenzetu. Lakini tujiulize Je, ni lazima tuwe na marafiki? Je tunaweza kuishi bila marafiki? Kwa hakika tunahitaji kuwa na marafiki katika maisha yetu kwa sababu ndiyo wanaotupenda na kutujali. Ni washirika wetu katika raha na shida, furaha na huzuni, tabu na raha, njaa na shibe, umaskini na utajiri, ugonjwa na afya na pengine hata katika uzima na kifo na mengineyo mengi. Husemwa kuwa na marafiki wema na wa kweli hushinda kuwa na mali.

 Lulumaines na Mayness

 Oliva na Mayness
Rafiki ni mtu yeyote ambaye mnakubariana kuishi kwa kushirikiana mambo mbalimbali ikiwa ni ya furaha ama ya huzuni. Rafiki anaweza kuwa mtu yeyote na wa lika yeyote ingawa watu wengi hupenda kuwa na rafiki wa lika moja na jinsia moja. Kwa hali ya kawaida hata wazazi au ndugu yako yeyote anaweza kuwa rafiki yako.

Kwa kawaida rafiki huwa mtu wa kwanza kujua matatizo au shida yoyote ambayo unayo. Na siku zote rafiki hujua siri zako nyingi kuliko mtu yeyote kuliko wazazi, mume/mke au hata ndugu yako. Hivyo rafiki ni bora kuliko kitu kikingine chochote. Vilevile rafiki huyu anaweza kukusababisha kuingia katika matatizo au kukusaidia kukuondoa katika dimbi la matatizo kwani rafiki ni mshauri mkuu katika maamuzi yako yeyote unayofanya. Leo tena nimependa kuongea habari hizi kwani zimekua zikigusa sana maisha yetu ya kila siku.
Je ni kwanini tunakuwa na marafiki?
Binafsi ninafahamu rafiki ni mtu wa kwanza kumweleza shida na matatizo yangu hivyo huwa ni muhimu kuwa naye ili tu kumpata mtu wa kunifariji katika mambo hayo na kunishauri pia. Watu wengi hulazimika kuwa na marafiki ili tu wapate watu wa kuwashauri katika mambo yao, unawaweza kuwa na marafiki wengi lakini lazima huwa yupo mmoja ambaye mnaweza kushirikiana na kusaidiana katika shida na raha na ambaye mnaweza kushirikishana mengi kuliko mtu mwingine. Yafuatayo ni baadhi ya mambo yanayo mfanya mtu alazimike kuwa na Rafiki/Marafiki.
Zitha, Ruth na Mayness

1. Upweke
Watu wengi wakiwa katika hali ya upweke hulazimika kuwa na marafiki ili tu waweze kukabiliana na hali hiyo. Upweke unaweza kutokana na mambo mengi mfano kuondokewa na mwenza mke/mme. Au kwa wale walio katika mahusiano kuacha/kuachika na wenza wao, pia upweke unaweza kuwa hata baada ya kuondokewa na ndugu au familia eitha kwa kufariki au tu kuwa mbali na upeo wa macho yako. Hali hizi zinaweza kumfanya mtu kutafuta faraja na kulazimika kutafuta rafiki anayeweza kusimama badala ya mambo yote hayo.

2.  Ushauri
Kunawakati tunalazimika kuwa na marafiki/rafiki kwasababu tu tunatafuta washauri katika shughuri zetu mbalimbali. Tunaamini rafiki anaweza kuwa mshauri na kukufanya mambo yako yaende sawia.

Yapo mambo mengi yanayoweza kumfanya mtu awe na rafiki/marafiki katika maisha ya kawaida . Usitafute marafiki wengi, tafuta marafiki wa kweli. Ni vizuri kujua watu wengi, lakini hata katika kikundi cha watu wengi, unajihisi huru zaidi kunapokuwa na watu wachache unaoweza kuwasiliana nao kwa uhuru. Hivyo tafuta rafiki wachache mnao endana ili tu muende sawa.
 Thea na Mayness
Rafiki wa kweli ni yupi na je uliyenaye ni rafiki wa kweli?
Ni yule mnaye endana katika mambo na maswala yenu tofauti tofauti. Marafiki wengi hupenda kuenda kwa Lika, vipato vyao, maisha yako, elimu yao, tabia zao  na wakati mwingine hata mwonekano wa nje. Watu wengi hawajui kuwa urafiki unaweza kuwa zaidi ya ndoa, mme/mke. Rafiki sahihi ni yule tu anayechukulia mapungufu yako. Rafiki wa kweli pia hukurekebisha pale tu unapokosea na kukuweka katika njia salama. Rafiki wa kweli anaweza kuwa hivi:-

1. Ana upendo wa dhati kwako.
Upendo ni jambo dogo sana lakini hubeba uzito mkubwa sana katika urafiki. Kupendwa na rafiki yako ni raha sana wapendwa. Upendo haupimwi kwa kuletewa zawadi tu hapana upendo wa dhati uingia kwenye mambo mengi ikiwa kusaidiana katika raha na shida. Rafiki mwenye upendo wa dhati hakuachi wakati wa shida, huwa karibu nawe wakati wowote. Hukushauri kufanya maamuzi ya busara na hekima wakati wote. Hukuzuia kufanya mabaya na hukuepusha kuingia katika matatizo.
 Mayness na Elithabeth (Liz)
2. Huchukulia mapungufu yako
Kila binadamu anamapungufu yake, hivyo rafiki husoma mapungufu ya mwenzake na kumchukulia kulingana na pungufu hilo alilonalo. Ingawa kunawakati mwingine inakera sana unakuta umemwambia pungufu lake na kumtaka ajaribu kujirekebisha lakini hakuelewi. Hivyo hapo uvumilivu unatakiwa pia. Rafiki wa kweli hakuongelei pungufu lako kwa mtu mwingine hukaa chini na kujadiri jinsi ya kukusaidia katika tatizo/pungufu hilo.

3. Hukushirikisha katika mambo yake
Ushirikishwaji ni jambo linaloweza kudumisha urafiki. Kwa mfano umekua ukifikiri kufanya jambo fulani la maendeleo. Nina amini rafiki anaweza kuwa mtu wa kwanza kumshirikisha katika hilo. Mfano bwana nimepata Mchumba, rafiki anaweza kuwa mtu wa kwanza kupata taarifa hizo. Ingawa urafiki wa sikuizi umekua mgumu sana unaweza kumshirikisha kitu yeye akajikuta kinamchukiza na asiseme kitu, huo si urafiki wa kweli. Rafiki wa kweli hushirikishana na kushirikiana katika mambo yao.

4. Hufurahia maendeleo yako
Rafiki wa kweli hufurahi pale unapoendelea kwa kila jambo pasi na kukuonea wivu. Mfano mdogo umebahatika kupata kipato kidogo na kujenga kibanda unapomshirikisha rafiki yako anatakiwa afurahi na kukuuliza mbinu ulizotumia ili naye ajifunze na si kwakuona wivu. Urafiki mwingi huvunjika katika mazingira kama haya.
 Twilumba, Mayness na Elina wakibadirishana mawazo


Ili uanzishe urafiki mzuri lazima nyote wawili mwe na viwango sawa. Yaani rafiki yako anapaswa kufuata kanuni kama zako kuhusu mambo ya kiroho na ya maadili. Jambo la pili ni kuwa na sifa zinazofanana, lakini hilo halipaswi kuwa jambo kuu. Na jambo linalofuata ni kuwa na mapendeleo (Hobbies)  yanayopatana, lakini hilo si jambo la maana sana. Unaweza kuwa rafiki ambaye ana mapendeleo yenu na vipawa vyenu vipo tofauti lakini mkawa na upendo wa dhati. 
 Mayness na Samiwath wakiwa Ruaha National Park

Ukiona hamwendi sawa na rafiki uliye naye jua huyo si saizi yako, Mfano:- 

  • Unaweza kujikuta ukimshirikisha mambo mengi unayofanya lakini yeye hafanyi hivyo jua huyo si rafiki sahihi.
  • Rafiki ambaye anaweza kukukasirikia bila sababu ya msingi na bila kukueleza jua huyo si sahihi kwako. 
  • Rafiki anayeweza kukuongelea mabaya yako kwa watu wengine jua si zaizi yako. 
  • Rafiki anayefurahia wewe unapopatwa na shida hachukulii tatizo lako kama ni lake pia huyo si sahihi kwako tena mkimbie kabla mambo hayajaharibika. 
  • Rafiki anayeshindwa kukupongeza pale unapofanya zuri na kukukosoa unapokosea huyo si sahihi.

Rafiki anatakiwa kuwa mtu wa kwanza kuchangia maendeleo yako na kuwa mshauri mkubwa kwa kila unachokifanya.


 Imakulatha na Mayness



MWISHO NITOE ANGALIZO
Pamoja na ukweli kwamba rafiki ni muhimu katika maisha, usipokua makini na uchaguzi rafiki huyo huyo anaweza kuwa Sumu katika maisha yako, unaweza chambua kuona kumbe baadhi sio rafiki, ni maadui. Ni jambo zuri sana kuwa na rafiki, na rafiki ni muhimu sana. Hata hivyo, ni jukumu lako kusimamia vema urafiki wako na watu wengine. Haitoshi tuu kuwa na rafiki wema, bali unapaswa kujua namna ya kuishi na hao rafiki wema. Endelea kuwa na maamuzi binafsi, tafuta uhuru wa fikra na usiogope kuwa na mtazamo tofauti na rafiki zako. Kumbuka Kwa hakika, hakuna kitu kinachojenga urafiki kama kutendeana mema, na rafiki wa kweli hakuzungumzii mabaya yako kwa watu.
 Edna na Mayness

Mimi ninawapenda sana rafiki zangu na wengi wao wamekua msaada kwangu. Mungu aendelee kuwapa maisha marefu Amina.