Mashabiki wa Simba TZ wazua vurugu
Polisi jijini Dar es Salaam Tanzania wamelazimika
kutumia Mabomu ya machozi kuwatawanya mashabiki wa Klabu ya Simba,baada
ya kumalizika mechi ya Ligi kuu soka Tanzania bara siku ya Alhamis
ambapo Simba ilitoka sare ya kufungana bao 1-1 na timu ya Kagera Sugar.
Vurugu hizo zimezuka mwishoni mwa mechi ambayo
timu ya Simba imezidi kuporomoka hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa
ligi hiyo kufuatia matokeo ya sare ya bao 1-1.Simba ilianza kuliona lango la Kagera Sugar katika dakika ya 45 baada ya mshambuliaji raia wa Burundi Amis Tambwe kufunga bao la kwanza lililodumu hadi mapumziko.
Katika Kipindi cha pili Simba walianza kucheza kwa kujihami hali iliyosababishga Kagera kukaribia lango lao mara kwa mara na hatimaye wakafanikiwa kusawazisha katika dakika ya 90.
Kwa matokeo hayo Simba imeporomoka hadi nafasi ya nne wakiwa na pointi 21,huku Azam, wakishika nafasi ya kwanza kwa kuwa na pointi 23 sawa na Mbeya City lakini wakitofautiana kwa magoli ya kufunga.
Yanga ni ya tatu kwa kuwa na pointi 22.
Herve Renard aaga Chipolopolo
Zambia imempa idhini kocha Herve Renard kuyaacha
majuku yake katika timu ya taifa ya nchi hiyo ili kuchukua jukumu lake
jipya la kuwa kocha wa timu ya ufaransa ya FC Sochaux.
Kocha huyo alikuwa ameanza muhula wa pili wa
mkataba wake kuwa kocha wa timu ya taifa ya Zambia mnamo mwezi Oktoba
mwaka 2011 na kuiwezesha Chipolopolo kufuzu kwa kombe la mataifa ya
Afrika miezi minne baadaye.Zambia sasa imempa kazi ya muda Patrice Beaumelle kuwa kocha wa Chipolopolo.
Beaumelle, amekuwa akifanya kazi kama kocha wa muda, na atashikilia wadhifa wa kocha mkuu wakati Chipolopolo watapocheza mechi ya kirafiki na Brazil mjini Beijing tarehe 15 Oktoba.
Shirikisho la soka nchini humo katika taarifa yake lilisema kuwa kocha "Herve Renard ameachishwa majuku yake ili kumruhusu kuiongoza timu ya Ufaransa.''
Renard, mwenye umri wa miaka 45, alichukua wadhifa huo wa kuwa kocha wa timu ya taifa ya Zambia mwaka 2008 na aliiongoza timu hiyo hadi kufika robo fainali za kombe la mataifa ya Afrika mwaka 2010.
Baadeya alikuwa kocha wa timu ya Angola na USM Alger kwa muda kabla ya kurejea kuwa kocha wa Zambia na kutimiza ndoto yake ya kuiongoza Zambia kunyakua kombe la taifa bingwa Afrika mwaka 2012.
Kazi ya ujenzi katika Uwanja
Kazi ya ujenzi katika Uwanja utakaochezewa mechi za kombe la dunia la soka mwaka 2014 nchini Brazil zimesimamishwa baada ya jaji wa mahakama kusema kuna wasiwasi kuhusu usalama.
Aliamrisha ukaguzi mpya ufanywe kabla ya kuanza tena shughuli za ujenzi. Akiongeza kusema kumegunduliwa kasoro nyingi katika ujenzi huo.
Taarifa hizo zinakuja wiki moja tu baada ya uchunguzi kufichua kwamba wafanyikazi walioajiriwa katika ujenzi wa mradi mwingine wa kombe la dunia walikabiliwa na hali ya kitumwa.
Wachunguzi hao walisema pia kwamba zaidi ya wafanyikazi 100 walioajiriwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Sao Paulo wanaishi katika hali duni karibu na uwanja huo.
Mnamo mwezi wa Agosti, waziri wa michezo Aldo Rebelo alisema ana wasiwasi jinsi ujenzi ulivyochelewa katika viwanja vitano vya michuano ya kombe la dunia mwakani.
Baada ya ziara yake nchini Brazil, katibu mkuu wa FIFA Jerome Valcke,alisema viwanja vyote lazima viwe tayari ifikapo mwezi Desemba na kuonya hatavumilia tena kuchelewesha ujenzi na hakuna 'mpango mbadala'.
Michuano ya kombe la dunia imepangwa katika viwanja 12 nchini kote Brazil.
Na BBC Swahili
Is this yours
ReplyDeleteYes Anonymous whats wrong?
ReplyDelete