Njia 10 za kuimarisha kumbukumbu kichwani
Miongoni
mwa hazina muhimu kwa mwanadamu ni kuwa na uwezo wa kukumbuka vitu kwa
urahisi. Wanafunzi wengi hushindwa kufanya vizuri mitihani yao kwa
sababu ya kukabiliwa na tatizo la usahaulifu, ambao huchochewa na mambo mengi ukiwemo ulevi wa pombe, utumiaji wa dawa za kulevya na msongo wa mawazo ya kimaisha.
Licha ya uwezo wa
kumbukumbu kupungua kutokana na umri wa mtu, sayansi yaitegemei kijana
mwenye umri wa chini ya miaka 28 kukabiliwa na tatizo hili kwa kiwango
kikubwa, ingawa wale wenye miaka zaidi ya 40 wanatajwa kuzorota katika
uwezo wa kukumbuka mambo.
Hata
hivyo uchunguzi unaonesha kuwa watu ambao huzingatia suala la kanuzi za
afya zikiwemo mbinu za kukuza kumbukumbu ya akili hupunguza kwa kiasi
kikubwa mmeng�enyeko wa seli zinazojenga uwezo wa akili katika kutunza
kumbukumbu. (Susan Tapert mwanasaikolojia kutoka Chuo cha California San Diego na kituo cha VA San Diego nchini Marekani anathibitisha haya pia).
Hivyo
basi, ili mwanafunzi aweze kuwa na uwezo wa kutunza vema mambo
anayosoma na kufundishwa na waalimu wake darasani lazima aweze
kuiongezea akili yake uwezo wa kutunza kumbukumbu kwa kufanya yafuatayo:
1 . LISHE BORA
Ni
wazi kuwa wengi wetu tunafahamu maana ya lishe bora, lakini kwa mujibu
wa utafiti uliofanywa na Chuo cha American Academy of Neurology
kinachojihusisha na mambo ya neva, ulibaini kuwa machungwa, Spinachi,
Karoti, brokoli (aina fulani ya mboga kama kabichi), viazi vitamu na
mboga mboga huuongezea uhai ubongo na kumfanya mwanadamu asiweze
kushambuliwa na magonjwa wa kupooza.
Aidha
matunda na vyakula vyenye vitamini B, Foliki Asidi (folic acid),
Niasini (niacin) Kalkumini (curcumin) husaidia kuufanya ubongo uwe na
mawasiliano ya kutosha na viungo vingine vya mwili na kupunguza kwa
asilimia 11 uhalibifu wa seli ndani ya ubongo. (Utafiti wa National
Research Council nchini Milan, Italy unathibitisha kuwa vyakula vyenye Vitamini C na E hupunguza kiwango cha usahaulifu)
2. MAZOEZI YA MWILI
Ufanyaji
wa mazoezi ya mwili huimarisha misuli na kusaidia akili kuweza kufanya
kazi vema, hii inatokana na ukweli kwamba tunapofanya mazoezi tunakuwa
tunaongeza msukumo wa damu mwilini na hivyo kuufanya ubongo kufikiwa na
damu ya kutosha ambayo ni muhimu kwa uimara wa kumbukumbu.
Mara nyingi, mazoezi
yanayofaa zaidi kwa afya ya mwili na uimarisha wa ubongo ni yale ya
asubuhi na jioni. Kuhusu aina ya mazoezi inategemea na umbo la mtu,
lakini kukimbia, kuruka kamba, kucheza mpira na hata kuinua vitu vizito
vinavyolingana na uwezo wa mtu ni bora kwa afya. Mazoezi ya aina hii
yakifanywa na wanafunzi yanaweza kuwasaidia pia kutunza kumbukumbu za
masomo wanayofundishwa.
3 : MAZOEZI YA AKILI
Ni
muhimu kwa mwanafunzi kuwa na mazoea ya kuifanyisha akili yake mazoezi
ya kutunza kumbukumbu kwa kuingiza kichwani mambo ambayo hakuyazoea na
kuyafanyia mazoezi ya kuyakumbuka. Kwa mfano mwanafunzi anaweza kundika
namba zisizopungua 14 na kuanza kuzitaja kwa kufuta mpangilio
aliojiwekea.
Namba
zinatakiwa ziandikwe kwa kuchanganywa si kwa kuzifuatanisha kwa mtindo
wa kuhesabu. Mfano, 23938393835575, baada ya kuziandika kwa mfumo huo
mwanafunzi atatakiwa kuzikariri kwa dakika tano kisha kufumba macho au
kutazama pembeni na kuanza kuzisoma kwa kufuata mfululizo huo, huku
akihakikiwa na mtu mwingine. Mazoezi haya yatamsaidia kuondoa tatizo la
kusahau na kumpa kipimo ni kwa kiwango gani hana uwezo wa kukumbuka.
Endapo
mwanafunzi atashindwa kufikia kiwango cha zaidi ya nusu ya namba
alizojiwekea afahamu kuwa ana uwezo mdogo wa kutunza kumbukumbu hivyo
anatakiwa kuongeza juhudi za kujiimarisha.
Njia nyingine ya kuifanyisha mazoezi akili ni kujifunza mara kwa mara mambo mapya, ikiwa ni pamoja na kuimba nyimbo kwa lugha
ya kigeni, kujifunza lugha za makabila mengine, kutembelea mitandao
mbalimbali ya intaneti na kusoma, kucheza michezo ya kwenye simu na
kompyuta.
Aidha usomaji wa vitabu,
urudiaji wa mara kwa mara wa notisi za darasani, husaidia kuongeza
msukumo wa akili katika kutunza kumbukumbu kichwani. Hata hivyo tafiti
nyingi zinaonesha kuwa uhudhuriaji wa majadala na uongeaji wa mambo ya
msingi mbele ya watu wengi huimarisha uwezo wa mtu kukumbuka mambo kwa
urahisi.
4. UTUMIAJI WA VINYWAJI
Vinywaji
kama kahawa, chai nyeusi navyo huchangia kuongeza uwezo wa ubongo
kutunza kumbukumbu. Inashauriwa kwa mwanadamu kutumia walau kikombe
kimoja cha vinywaji hivyo ili kuongeza enzymes ambazo ni muhimu kwa kuuongezea nguvu ubongo ili uweze kutunza kumbukumbu. Hata hivyo vinywaji vikali kama pombe haviruhusiwi kwani huchangia kudumaza uwezo wa kukumbuka.
5. PUNGUZA MSONGO WA MAWAZO
Ubongo
unaweza kushindwa kutunza kumbukumbu endapo mtu husika atakuwa na
msongo wa mawazo yatokanayo na shida za kidunia. Endapo mwanafunzi
atakuwa mtu mwenye kuutumikisha ubongo wake katika mawazo yenye kuumiza
kila wakati, hawezi kuwa na uwezo wa kukumbuka anayofundishwa.
Hivyo
ni vema kupunguza mawazo kwa kuwashirikisha wengine magumu unayokutana
nayo maishani na kukubali kuyaacha yapite ili yakupe nafasi ya kuishi kama
wewe. Hatari ya msongo wa mawazo ni kuongeza kiwango cha seli za
cortisol ambayo huharibu ubongo wa kati ambao ni muhimu kwa kutunza
kumbukumbu.
6. KULALA
Watu wengi wakiwemo wanafunzi wamekuwa wakipuuza usingizi kwa kusoma sana usiku na kuacha kupumzisha miili yao kwa kulala, jambo ambalo hili ni hatari kwa utunzaji wa kumbukumbu kichwani.
Ifahamike kuwa usingizi ni kama
chujio la akili ya mwanadamu, ambapo mtu anapolala mchakato hufanyika
akilini kwa kuyachambua mamilioni ya mambo ambayo mhusika aliyaona,
kuyasikia, kuhisi na pengine kuyatenda. Mchakato huo huweza kuchuja
mambo mabaya na kuyatupa na mema huhifadhiwa kwenye kumbukumbu.
Hivyo, kama mwanafunzi hatolala, mambo yote yakiwemo ya kipuuzi aliyofanya mchana yatabaki kwenye akili yake na kama mtindo huo wa kutolala utaendelea unaweza kuufanya ubongo uchoke na kupoteza kumbukumbu ya mambo muhimu yakiwemo ya shuleni.
Utafiti uliofanywa mwaka 2008 na Chuo cha Pennsylvania
ulionesha kuwa wanafunzi wanaolala kwa saa 6 kwa siku huwa na
kumbukumbu nzuri zaidi ya wale wanaolala kwa kiwango cha chini ya saa
hizo. Utafiti wa aina hii ulifanywa pia na Chuo Cha Luebeck na
kubainisha kuwa akili huongezewa uwezo mara tufu kwa kutunza kumbukumbu
pale mtu anapokuwa analala usingizi mnono.
7. TUMIA MUZIKI
Muziki
unatajwa kuwa na faida katika kumsaidia mtu kukumbuka mambo yaliyopita,
inawezekana kabisa kwa kupita wimbo ukakumbuka mambo ambayo uliyafanya
siku za nyuma. Hivyo kuufurahisha mwili kwa kucheza muziki, kusikiliza
nyimbo, kunaweza kuongeza uwezo wa mtu kukumbuka mambo. Hata hivyo
kujifunza lugha au jambo fulani kwa njia ya wimbo ni rahisi kukumbuka
kuliko kuhifadhi maneno yenyewe.
8. KUANDIKA
Ni
muhimu kwa mwanafunzi kuwa na kumbukumbu za pembeni nikiwa na maana ya
maandishi ya mkono. Ni muhimu kuorodhesha mambo ambayo umekusudia
kuyafanya au yalikutokea kwa kuyaandika kwenye kitabu kidogo cha
kumbukumbu. Mfano, unaweza kuandika siku uliyoanza shule, uliyozaliwa,
tarehe uliyomaliza darasa la saba n.k.
9. ONDOA HOFU
Kuna
wanafunzi wengine hushindwa kukumbuka mambo si kwa sababu akili
imesahau, bali wanajichanganya kwa hofu na kutojiamini kwamba
wanachokumbushwa na akili kwa wakati huo kiko sahihi. Hivyo ni wajibu wa
mtu kujiamini na kutupilia mbali wasi wasi wote unaojitokeza wa kuhofu
kuchekwa au kutofanya vizuri katika jambo lililopo mbele yake.
10. AFYA
Jambo
la mwisho ambalo ni muhimu katika uimarishaji kumbukumbu za kichwani ni
mtu kuwa na afya kwa maana ya kuhakikisha kuwa anatibiwa magonjwa yake
na anakuwa mfuasi mzuri wa huduma za kitabibu kwa ajili ya kuuwesha
mwili wake ufanye kazi kama unavyokusudia.
No comments:
Post a Comment