- Kabla ya kutokea vurugu hizo, mashabiki pia walifanya vurugu Mbeya baada ya kumalizika kwa pambano la Ligi Kuu kati ya Mbeya City na Prisons zote za jijini humo.
Katika pambano la Ligi Kuu ya soka Bara kati ya
Simba ya Dar es Salaam na Kagera Sugar ya Bukoba lililofanyika kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam vurugu kubwa zilitokea.
Kabla ya kutokea vurugu hizo, mashabiki pia
walifanya vurugu Mbeya baada ya kumalizika kwa pambano la Ligi Kuu kati
ya Mbeya City na Prisons zote za jijini humo.
Vurugu za Dar es Salaam zilitokea dakika za mwisho
za mchezo uliofanyika Alhamisi iliyopita wakati Kagera Sugar ilipopata
penalti dakika za majeruhi za mchezo huo.
Wakati Simba ikiongoza kwa bao 1-0, mwamuzi aliipa
Kagera Sugar penalti ambayo iliipatia timu hiyo goli la kusawazisha
ambalo liliwafanya mashabiki wa Simba waanze vurugu kwa kuvunja viti na
kuvitupa uwanjani.
Bila ya kujali uhalali au uharamu wa penalti hiyo,
tunapinga hatua iliyochukuliwa na mashabiki wanaoaminika kuwa ni wa
Simba kwani mwamuzi ndiye mwamuzi wa mwisho mchezoni. Uamuzi wa mwamuzi
katika mpira wa miguu yanapaswa kukubaliwa na kila aliye uwanjani kwani
huo ndiyo utaratibu wa mchezo huo na si vinginevyo.
Ni lazima klabu zitafute njia mwafaka ya
kuwasilisha malalamiko iwapo wanahisi kuwa waamuzi kwa njia moja au
nyingine hawakuchezesha vizuri na si kujichukulia uamuzi.
Tatizo la waamuzi nchini linapaswa lifuate mkondo
mzuri katika kulitafutia ufumbuzi na halitaweza kwisha kwa mashabiki
kuchukua hatua mkononi au kufanya vurugu.
Katika vurugu hizo, polisi walifyatua mabomu ya
kutoa machozi hali iliyofanya jukwaa lilikuwa na mshabiki waliokuwa
wanafanya fujo kuwa mbaya na kwa hiyo kuhatarisha maisha ya watu hasa
walemavu ambao hawakuwa na uwezo wa kukimbia.
Hili ni jambo la hatari kubwa kwani yanaweza
kutokea maafa kama ilivyowahi kutokea katika nchi zingine duniani
zikiwemo za Afrika.
Kila mmoja ni lazima aelewe kwamba Tanzania
inaweza kukumbwa na maafa iwapo vurugu za aina hii zitatawala katika
viwanja vya soka nchini.
Kuna umuhimu mkubwa kwa viongozi wa klabu
kuwaelimisha mashabiki wao kuwa wavumilivu wanapokuwa viwanjani ili
kuhakikisha michezo inamalizika kwa usalama.
Inapaswa ieleweke kwamba michezo ni furaha na
lengo lake kuu ni kujenga uhusiano nzuri baina ya wanamichezo na si
kuleta uhasama.
No comments:
Post a Comment