Monday, November 4, 2013

Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini, Dk Sengondo Mvungi amejeruhiwa na watu wanaosemekana kuwa majambazi usiku wa kuamkia jana

Rais Jakaya Kikwete (wa pili kushoto) akiwa na mkewe Mama Salma pamoja na Mwenyekiti wa chama cha NCCR- Mageuzi James Mbatia, na daktari wa zamu wakimwangalia mjumbe wa tume ya mabadiliko ya katiba, Dk Sengondo Mvungi, aliyelazwa katika taasisi ya mifupa Muhimbili (MOI) jana, baada ya kujeruhiwa na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi.

Kwa ufupi
Dk Mvungi, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Katiba, Sheria na Haki za Binadamu wa NCCR-Mageuzi aliwahishwa kwenye Taasisi ya Mifupa Hospitali ya Muhimbili (MOI), ambako amelazwa katika wodi maalumu huku hali yake ikiwa mbaya.

Dar es Salaam. Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini, Dk Sengondo Mvungi amejeruhiwa usiku wa kuamkia jana, baada ya kukatwa kwa mapanga na watu wasiojulikana waliovamia nyumbani kwake Mpiji-Magohe, jijini Dar es Salaam.
Dk Mvungi, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Katiba, Sheria na Haki za Binadamu wa NCCR-Mageuzi aliwahishwa kwenye Taasisi ya Mifupa Hospitali ya Muhimbili (MOI), ambako amelazwa katika wodi maalumu huku hali yake ikiwa mbaya.
Taarifa kutoka kwa ndugu na watu waliomtembelea hospitalini hapo wanasema kwamba hali ya Dk Mvungi ni mbaya kwani alikuwa hawezi hata kuzungumza.
Akisimulia tukio hilo, dereva wa Dk Mvungi anayeitwa Emmanuel Ntaro, alisema akiwa nyumbani kwake majira ya saa 6:30 usiku, alisikia mlipuko mkubwa kisha zikasikika kelele zikitokea nyumbani kwa bosi wake.
“Nilifika na kukuta hajitambui, tukampeleka Hospitali ya Tumbi Kibaha mkoani Pwani alikopatiwa huduma ya kwanza kabla ya kumpeleka MOI ambako anaendelea kuchunguzwa na kupatiwa matibabu,” alieleza Ntaro
Alisema kuwa watu wapatao sita, walivamia nyumbani kwa Dk Mvungi ambako baada ya kuvunja mlango na kuingia ndani, walimjeruhi kwa kutumia mapanga huku wakidai wapatiwe fedha. Watu hao walimsababishia majeraha usoni, kichwani na sehemu nyingine za mwili.
Akizungumza na Mwananchi jana, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema mbali na kupata matibabu MOI, pia walilazimika kumpeleka Hospitali ya Aga Khan kwa ajili ya vipimo zaidi katika mashine ya CT Scan kama walivyoshauriwa na madaktari wa zamu.
Mbatia alisema kuwa baada ya Dk Mvungi kufanyiwa kipimo hicho alirudishwa tena MOI kwa matibabu na uangalizi maalumu. “Hali yake inaanza kuimarika tofauti na nilivyomuona saa nne asubuhi, “ alisema Mbatia muda wa saa 12 jioni jana alipozungumza na gazeti hili.
Alisema kwamba pia watu waliohusika na tukio hilo waliiba kompyuta mpakato (laptop) pamoja na bastola ya Dk Mvungi.
Kamanda wa Mkoa wa kipolisi Kinondoni, Cammilius Wambura alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
“Kweli hilo ni tukio la kihalifu na sisi tunaendelea kulifanyia kazi. Tunawahakikishia Watanzania kuwa watu hao watapatikana na kufikishwa kwenye mkono wa kisheria,” alisema.
Kilichotokea

No comments:

Post a Comment