“Nilifika na baba hapa alinichukua toka Mwanza akaniambia ananileta kwa shangazi anayeishi hapa kuja kusoma” anasema Cosmas.
Hebu tafakari, kijana wa miaka 12
ambaye hajawahi kufika jijini Dar es Salaam, anafika Ubungo kwa mara ya
kwanza akiwa na baba yake, na ghafla wanapotezana.
Hii ilimtokea kijana, Cosmas Steven,
13 ambaye alifika hapa jijini mwezi Januari akitokea Mwanza yeye pamoja
na baba yake. Baada tu ya kufika katika kituo cha mabasi yaendayo
mikoani cha Ubungo, Cosmas alipotezana na baba yake.
“Nilifika na baba hapa alinichukua toka Mwanza akaniambia ananileta kwa shangazi anayeishi hapa kuja kusoma” anasema Cosmas
Kwa bahati mbaya, Cosmas hakuweza
kumpata baba yake na matokeo yake, aliishia kuishi katika mitaa ya jiji
la Dar es Salaam ambapo kwa sasa anaishi kwa kuuza chupa tupu za maji na
kucheza kamari.
Cosmas ambaye ameishia darasa la sita
anasema: “Natamani kurudi nyumbani na kumuona baba yangu lakini sielewi
namna ya kumpata, nnachojua ni kuwa anaitwa Steven John”
Cosmas pamoja na watoto wengine wa
mitaani katika eneo hili wanaishi maisha yasiyo na utofauti na wanyama.
Wanaoga katika Mto wa Msimbazi nyakati za usiku wakati watu wote
wamelala.
Wanalala katika vibaraza vya maduka
katikati ya jiji ambapo hata hivyo hutakiwa kuchangia gharama ya malazi
ya shilingi 200 hadi 300 kwa usiku mmoja.
Chanzo chao kikuu cha mapato ni
kuuza chupa tupu zinazozagaa kwa wenye viwanda na kampuni ambazo
zinanunua chupa hizo kwa kilo na kucheza kamari au kuombaomba pembezoni
mwa barabara.
Hata hivyo, fedha hizo wakati
mwingine huenda zisiwe riziki kwao kwani usiku wanapolala vibaka au
watoto wa mitaani wenye nguvu zaidi yao, huwanyang’anya kwa nguvu fedha
hizo.
Haya ndiyo maisha ya watoto wa
mitaani ambapo si Cosmas pekee bali lipo kundi kubwa la vijana
wanaoishi mitaani Tanzania nzima.
Tovuti ya Humanium Help the
Children(HHC) inaeleza kuwa katika Jiji la Dar es Salaam pekee kuna
watoto 3,000 hadi 5,000 ambao wanaishi mitaani.
Pia tovuti hiyo inaeleza kuwa watoto
hao wengi wao wana umri wa kuanzia miaka mitano hadi 18 ambapo asilimia
80 kati yao ni wanaume wenye umri wa miaka saba hadi 14.
Mkurugenzi wa Elimu kwa Watoto,
kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto,(Unicef) Dk
Victoria Masabo anasema tatizo la watoto wa mitaani linaendelea kuwa
kubwa na gumu kwa sababu kadhaa ikiwemo wazazi na walezi.
“Wazazi na walezi ndiyo watu wa
kwanza wanaotakiwa kuhakikisha kuwa mtoto anaishi salama, kuhakikisha
yupo wapi na anafanya nini,’ anasema
Anasema talaka, kuvunjika kwa familia na migogoro ndicho chanzo kikubwa kinachosababisha ongezeko la watoto wa mitaani.
Anashauri kuwa taasisi zitafute njia
mbadala kuhakikisha kuwa watoto wa mitaani wanapata maeneo maalumu kwa
ajili ya watoto hao na wahakikishe wanakaa katika maeneo hayo, wanapata
elimu hadi watakapokuwa watu wazima.
Dk Masabo anasema tatizo hili la
watoto wa mitaani lisipofanyiwa kazi basi taifa litazalisha wezi,
majambazi, makahaba na kizazi haribifu.
Ipo sheria Tanzania ambayo inaeleza
kuwa iwapo polisi atamkuta mtoto wa mitaani anayeonekana hana umiliki wa
wazazi, basi atatakiwa amchukue na kumpeleka katika taasisi.
Sheria ya watoto ya mwaka 2009
inakataza watoto kuzagaa mitaani na iwapo wataonekana mitaani basi
sheria hiyo inasema wanatakiwa kupelekwa kwa ofisa ustawi wa jamii.
Afisa ustawi wa jamii anatakiwa
afuatilie iwapo mtoto au watoto hao wana wazazi na kama hawana wazazi
basi watafutiwe wazazi mbadala na kama hao pia hawatapatikana basi
watoto hao wapelekwe katika vituo maalum au taasisi.
Kwa bahati mbaya, sheria hii
haifuatiliwi na wanajamii au hata na polisi watunza sheria, na matokeo
yake watoto wa mitaani wanakosa haki zao na furaha ya utoto wanayotakiwa
kuipata.